MBIO KUELEKEA MLIMA KILIMANJARO!!

Meneja wa bia ya Kilimanjaro George Kavishe.

Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Riadha mkoani Dar es Salaam (DAAA), kimeimwagia sifa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro kutokana na kuanzisha mbio za aina yake za kukimbiza bendera ya Taifa kutoka Dar es Salaam hadi kilele cha Mlima wa Kilimanjaro.
Bia ya Kilimanjaro ndiyo inayodhamini mbio hizo zinazoshirikisha wanariadha nyota zaidi ya 70 wanapokezana bendera kila baada ya kilomita kati ya kumi na 12.
Akizungumza mjini Chalinze wilayani Bagamoyo juzi, Katibu wa DAAA, Kapteni Mstaafu Lucas Nkungu alisema kwamba, Bia ya Kilimanjaro imekuja na kitu kipya na chenye kuongeza ladha katika riadha chini.
“Tumefarijika sana kwa Bia ya Kilimanjaro kuibuka na aina hii ya mbio ambazo mara nyingi tumekuwa tukizisikia au kuziona katika nchi za wenzetu waliopiga hatua katika riadha,” alisema Nkungu ambaye mkoa wake ulipewa jukumu la kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa mbio hizo zenye kauli mbiu ya “Fikisha Tanzania Katika Hatua za Juu”.
Nkungu aliyeibatiza Bia ya Kilimanjaro kuwa `Mwanamichezo wa Kweli’, alisema mbio hizo zitachochea ukuaji wa riadha na hivyo kuwa na nafasi nzuri ya kuwakomboa wanamichezo waliopo na wanaotarajiwa kujikita katika riadha.
Mbali ya kuanzisha kwa mbio za kukimbiza bendera ya taifa kuelekea kilele cha Mlima Kilimanjaro, Bia ya Kilimanjaro imekuwa mstari wa mbele katika kudhamini michezo nchini.
Bia hiyo, licha ya kuwa wadhamini wakuu wa klabu kongwe na maarufu zaidi katika soka nchini, Simba na Yanga, pia ni mdhamini wa muda mrefu wa mbio za kimataifa za Marathoni za Kilimanjaro na zile zinazoshirikisha wanariadha kutoka zaidi ya nchi 25 duniani.
Ndio wadhamini wa Tuzo za Muziki za Kilimanjaro. Imekuwa pia ikidhamini michuano ya mpira wa kikapu ya mkoani Dar es Salaam `RBA Kili’.
Naye Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe aliye katika msafara wa wanamichezo ulioanza juzi jijini Dar es Salaam, akizungumzia mbio za bendera ya taifa, anasema; “Hii ni namna pekee ya kufurahia na kujikumbusha mafanikio yetu ya kiwango cha juu, ndiyo maana kampeni hii inaitwa ‘Fikisha Tanzania Katika Hatua ya Juu Zaidi.’’
Safari ya kukimbiza bendera hiyo katika miji kadhaa kati ya Dar es Salaam na Moshi, mkoani Kilimanjaro inatarajiwa kufikia kilele Ijumaa.

You liked this post? Subscribe via RSS feed and get daily updates.

0 comments:

Post a Comment